Machweo bandani

Nimekimbia mbio za nyika
Nimekanyaga nge na nyoka
Nimekimbia jangwa na milima
Nimekimbia, ikinyesha, ukivuma.

Nimekwepa mishale na manati
Nimehepa bunduki kwa bahati
Nimeponea mawe ya umati
Nimejongea hata giza tititi

Nimejificha kama fungo
Nimelikinga jua kwa ungo
Nimejibanza kama panya
Nimeziba kila mwanya

Nimefungua kila mlango
Nimepangua kila mpango
Nimesambua kila ngoma
Nimeambua vingi viweo

Kumi na mbili kawika jimbi
Mie huyoo kima cha mbilimbi
Bandani mie huyo nimeingia
Kimbia kote kimbia penzi kigoni lakunyatia.

© Paul Mndima  June 28, 2017

https://mwalimu255blog.wordpress.com

Advertisements

One thought on “Machweo bandani

Comments are closed.